MWENYE MATUSI
Posted by Tabu Bin Tabu on November 10, 2011
Yako majina ya vitu, mengine yasiyotajwa,
Yashangaza kuna watu, wenye uovu kujawa,
Waona kuwa si kitu, ni kama wanaolipwa,
Thawabu yako motoni, sikia mwenye matusi.
Mtu sio hayawani, anatumia akili,
Kuboboka hadharani, huwa ni kwake katili,
Matusi siwe kinywani, kama lusu tafadhali,
Thawabu yako motoni, sikia mwenye matusi.
Mdomo wako ni moto, wewe mja nakwambiya,
Wanena mambo mazito, hutaki kuyawaziya,
Ulimi wako ufito, mwilini wateketeya,
Thawabu yako motoni, sikia mwenye matusi.
Katu hutokaa tuli, kwa kweli tumefahamu,
Wewe ni ndumakuwili, mdomo wako ni sumu,
Wafitini kwa ukali, na kuua kama pumu,
Thawabu yako motoni, sikia mwenye matusi.
Hauna wakati wako, na kazi kwako hauna,
Kinywani hauna mwiko, mpyaro unajivuna,
Pasipo masikitiko, sokoni hutukanana,
Thawabu yako motoni, sikua mwenye matusi.
Utamkacho laana, ulimi wako huchungi,
Na lusifa wafanana, u kama mvuta bangi,
Unaitana majina, visivyotajwa kwa wingi,
Thawabu yako motoni, sikia mwenye matusi.
© Tabu Bin Tabu
24-10-2011